Sunday, May 31, 2020
Swahili > Habari > Habari za kikanda > Mtibwa Sugar yaibuka kidedea Kombe la Shirikisho 2018.

Mtibwa Sugar yaibuka kidedea Kombe la Shirikisho 2018.

Fainali ya kombe la shirikisho nchini Tanzania-ASFC imehitimishwa siku ya jana, Jumamosi katika dimba la Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha, kwa timu ya Mtibwa Sugar kuibuka na ushindi wa magoli 3 kwa 2 dhidi ya walima Alzeti, timu ya Singida United .

Kikosi cha timu ya Mtibwa Sugar kabla ya mchezo kuanza-ASFC.

Mchezo huo uliokuwa wa kuvutia na wa ushindani mkubwa, ulishuhudiwa na maelfu ya wapenda soka nchini na kufanya uwanja wa Sheikh Abeid kufurika na kuzizima kwa shangwe . Walima miwa wa Turiani, timu ya Mtibwa Sugar ndio walioanza kupata goli la kuongoza kupitia kwa Salum Kihimbwa mnamo dakika 22, na dakika ya 37 , Issa Rashidi aliipatia Mtibwa goli la pili na kuwafanya kua mbele kwa goli 2 bila.

Singida United ilianza kuchomoa goli la kwanza kupitia kwa Salum Chuku na kisha kiungo Tafadwa Kutinyu kuipatia goli la pili, kunako dakika dakika ya 71 na kufanya ubao wa matokeo usomeke 2 -2 . Katika dakika za lala salama, Ismail Aidan, winga wa Mtibwa Sugar alihitimisha Karamu ya ushindi kwa kuipatia Mtibwa Sugar goli la 3 na kufanya matokeo kuwa 3 – 2 .

Kikosi cha timu ya Singida United kabla ya mchezo kuanza-ASFC.

Katika mchezo huo wa fainali ya kombe la shirikisho, mchezaji Rashid wa Mtibwa alizawadiwa kadi nyekundu mnamo dakika 81 baada ya kumchezea rafu kiungo wa Singida United, Deus Kaseke . Kwa matokeo hayo klabu ya Mtibwa Sugar imepata nafasi ya kushiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao .