Mwenyekiti wa kamati ya kuisaidia klabu ya Yanga kuvuka katika kipindi hiki cha mpito, Abbas Tarimba amesema kuwa watani wao wa kihistoria Simba hawana uwezo wa kung’amua vipaji vipya katika Soka na kuvisajili.
Tarimba ameyasema hayo baada ya watani wao kumsajili mshambuliaji wa Gor Mahia, Meddie Kagere ambaye awali Yanga ilihusishwa kutaka kumsajili ili kuimarisha kikosi chake kuelekea katika michuano ya kombe la Shirikisho la Afrika na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa na Simba, aling’aa katika michuano ya SportPesa Super Cup akiwa na klabu ya Gor Mahia ambapo aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kuzivutia klabu kadhaa za Tanzania zikiwemo Simba na Yanga.

Katika siku za hivi karibuni, Abbas Tarimba aliwahi kuzungumza kuwa yeye na kamati yake watakuwa wanafanya usajili wao kimyakimya ili kuwaficha watani wao wasiweze kujua ni wachezaji gani wamewasajili.