Shirikisho la soka nchini Tanzania- TFF, limewakutanisha waamuzi wa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Mtibwa Sugar na Singida United kwenye mkutano wa pamoja siku moja kabla ya mchezo ili kuondoa kasoro zilizojitokeza katika baadhi ya mechi za hatua za awali.

Katika mchezo wa fainali,mwamuzi wa kati ni Emmanuel Mwandemba, waamuzi wasaidizi ni Mohamed Mkono na Ferdinand Chacha , na mwamuzi wa akiba ni Jonesia Rukyaa. Waamuzi hao, wamekutana na timu zote mbili na kuelezana taratibu na kanuni za mechi hiyo ya fainali.
Katika mchezo wa nusu fainali kati ya Singida United na JKT Tanzania uliochezwa kwenye uwanja wa Namfua Singida, ulitokea utata juu ya kanuni ya mchezo, ambapo timu ya JKT Tanzania walidai kuambiwa mchezo ungeishia ndani ya dakika 90 na kwenda kwenye penati lakini Singida walidai wameambiwa mchezo unaenda hadi dakika 120.

Mkutano wa jana pia ulihudhuriwa na mtathmini wa waamuzi Charles Mchau na Kamishna wa mchezo huo Mulamu Ng’ambi. Mchezo huo wa fainali ya kombe la shirikisho utachezwa leo jijini Arusha na mshindi ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la shirikisho barani Afrika.