Maafisa nchini Tanzania wamewatia mbaroni watu watatu wanoshukiwa kuwapatia sumu simba tisa katika mbuga ya taifa ya Serengeti. Vyombo vya habari vimesema, maafisa wa mbuga hiyo waligundua mizoga ya simba hao wikiendi iliyopita. Simba saba waliuawa katika tukio lingine kama hilo, katika mbuga hiyo hiyo mwaka wa elfu mbili na kumi na tano.

Polisi mkoani Mara Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, inasema watuhumiwa watatu waliokamatwa watafikishwa mahakamani baada tu ya upelelezi kukamilika.
Mbuga ya wanyama ya serengeti ndio kongwe na kubwa zaidi nchini Tanzania ikiwa na zaidi ya kilomita elfu 14 huku kwa mwaka ikikadiriwa kuwa na watembeleaji zaidi ya laki tatu na 50.