Saturday, May 30, 2020
Swahili > Habari > Madhila wanayopata wakimbizi wa Burundi kambini

Madhila wanayopata wakimbizi wa Burundi kambini

Madhila wanayopata wakimbizi

Burundi ni moja ya nchi maskini duniani na vita vya zaidi ya muongo mmoja vimeiacha nchi hiyo katika hali ya kutokua na utulivu kabisa.

Ukosefu wa amani nchini humo na taharuki ya uchaguzi wa mwaka 2015 uliosababisha maandamano ya wiki kadhaa yameathiri uchumi wa nchi hiyo na kuwaacha raia wake katika hali mbaya zaidi kuliko ile waliokuwa nayo mwanzoni.

Maelfu ya raia wa Burundi waliacha makazi yao kwa kuhofia vurugu na kukimbia katika nchi jirani hasa Tanzania na Rwanda.

Tanzania hivi sasa ina zaidi ya wakimbizi 110,000 kutoka Burundi katika kambi mbili, Nyarugusu na Nduta, ambazo zimefunguliwa hivi karibuni kupunguza msongamano. Wakimbizi zaidi wamekuwa wakiongezeka kila siku huku mashirika ya kutoa misaada yakikabiliwa na hali ngumu ya jinsi ya kugaw rasilimali chache walizonazo.

Miongoni mwa mashirika hayo ni kama lile la Oxfam ambalo limekuwa likifanya kazi nchini Tanzania tangu mwaka 2015. Shirika hilo limekuwa likijishughulisha zaidi katika miradi ya maji na usafi wa vyoo kwa wakimbizi hao wanaoishi katika kambi ya Nyarugusu na Nduta, zilizopo mkoani Kigoma, magharibi mwa Tanzania.

Ingawa maelfu ya wakimbizi hao hivi sasa wanapata maji safi na huduma muhimu za vyoo, lakini maisha katika kambi zenye msongamano na rasilimali chache sio rahisi. Hawa ni baadhi ya wakimbizi wakisimulia maisha ya kambini:

Kama ilivyo kwa raia wingi wa Burundi, Irakunda alilazimika kukimbia na mume wake na mtoto wao kutokana na sababu za kiusalama.

Baada ya kufika nchini Tanzania, yeye na familia yake walihamishwa katika kambi ya Nyarugusu kwa usafiri wa basi. “Tulikaa katika hema la pamoja kwa muda wa mwezi mmoja kabla kuhamishwa katika hema la famiia.” Hata hivyo, hema hilo haliwalindi dhidi ya chochote. Msimu wa mvua kali ndio inakuwa taabu kabisa. “Mvua ikinyesha usiku, hatulali. Inabidi tusimame pembezoni mwa hema letu mpaka mvua iache kunyesha. Siwezi kupika mvua inaponyesha, kwa hiyo tunakaa na njaa mpaka iishe.”

Wakati mwengine, hata kama hakuna mvua, upatikanaji wa kuni nao ni tatizo. Hata vyombo vya kupikia ni taabu kupata. Mgao wa chakula nao ni mdogo, kwa hiyo mara nyingi tunakaa bila kula. Licha ya hayo yote, Irakunda anashukuru kwa msaada wa chakula wanachopata.

“Natamani ningekuwa na fedha za kununua chakula ili nipate lishe nzuri. Afya ya familia yangu sio nzuri sana.” anasema Irunda, huku akielezea jinsi alivyopoteza baiskeli mpakani. Bila kuwa na usafiri, ni vigumu hata kupata kazi, hivyo kwa sasa wanategemea chakula cha msaada.

Hakizimana alirudi nyumbani kutoka shule na kukuta watu wote hawapo nyumbani. “Nilikuja Tanzania tarehe 10 mwezi Oktoba mwaka 2015. Nilitaka kutafuta familia yangu, lakini kwa bahati mbaya, alijikuta pekee yake katika kambi ya Nduta, huku mamake akiwa Nyarugusu. Amepewa hema ambalo anaishi na wanaume wengine sita.

Wakimbizi wa Burundi
Hakizimana alikuja kambini akitarajia kukutana na familia yake, lakini hakufanikiwa. Picha-Oxfam,

Kwa wanaume ambao wapo katika hali yake, anasema, “Mara nyingi changamoto ni kwamba, wanawake ndio wanapewa kipaombele na mashirika ya kutoa misaada. Hii inasaidia kwa wale wanaokuja kama familia, lakini katika mahema ya wanaume watupu, maisha ni magumu.”

Makala hii imetafsiriwa kutoka mtandao wa Oxfam International