Baadhi ya wabunge waliounga mkono mabadiliko ya katiba ya kuondoa kipengele cha ukomo wa umri wa urais nchini Uganda wameanza kukumbana na hasira kali za wananchi.
Takribani wabunge watatu wamekumbwa na vitendo vya kudhalilishwa tangu mbunge wa Igara Mashariki, Raphael Magyezi kuwasilisha bungeni muswada wa kuondoa ibara ya 102(b) ya katiba ya nchi hiyo inayoweka ukomo wa umri wa mtu kuwa rais ambao ni miaka 75.
Hatua hiyo inatazamwa kama jaribio la wabunge wa chama tawala, National Resistance Movement (NRM), la kumuwezesha rais Museven kukaa madarakani mpaka kifo.
Kwa upande wao, wabunge wa upinzani walipinga muswada huo, hatua iliyozua vurugu ndani ya bunge na hivyo makachero kutoka kikosi maalumu cha ulinzi wa rais kulazimika kuingilia kati na kuwaondoa wabunge hao wa upinzani.

Uamuzi huo wa bunge wa kujadili muswada umeamsha hasira kutoka kwa wananchi na wanaharakati wa vyama vya kiraia na baadhi yao wameanza kujichukulia sheria mkononi.
Ijumaa iliyopita, wananchi wa wilaya ya Mityana waliwatupia mawe wabunge wao wawili, mbunge wa jimbo la Mityana kwa upande wa wanawake Judith Nabakooba na mwenzake wa jimbo la Mityana kusini, Godfrey Kiwanda jambo ambalo liliwalazimu wabunge hao kukimbia.
Wapiga kura waliaanza kuwatupia mawe wabunge hao walipowasili katika mji wa Kiyoganyi ambako walifika kwa ajili ya kuunga mkono miradi ya maendeleo.
Kiwanda ambae pia ni waziri wa utalii alikuwa wa kwanza kuwasili katika eneo hilo.
Wananchi hao wenye hasira walianza kumtupia mawe Kiwanda wakati anashuka kwenye gari, hali ambayo ilimfanye awashe gari na kuondoka.
Dakika chache baadae, Nabakooba alielekea kwenye uwanja huo na kuishia kutupiwa mawe. Vijana waliokuwa wakiwatupia mawe wanasema wabunge hao hawatakiwi kwa kuwa wameivuruga katiba.
Katika hatua nyingine, akiongea na redio CBS, Nabakooba alisema vijana hao walilipwa ili kuwaharibia shughuli yao.
“Inasikitisha sana vijana wetu wanaweza kukubali kutumiwa,” alisema Nabakooba.
Pia alidai kuwa vijana hao wamesafirishwa kutoka eneo lingine ili kwenda kuvuruga shughuli yao.
Katika tukio lingine, James Kakooza, mbunge wa jimbo la Kabula katika wilaya ya Lyantonde aliponea chupuchupu kuuawa na waombolezaji huko wilayani Lwengo kwa kuwa nae alikuwa sehemu ya wabunge waliounga mkono mabadiliko ya katiba.
Hali hiyo ilitokea wakati Kakooza alipowasili wilayani Lwengo kushiriki mazishi ya baba wa mbunge mwenzake wa jimbo la Masaka, Mathias Mpuunga.
Waombolezaji walimzomea mbunge huyo na kumtaka kuondoka mara moja, wakimwambia kuwa hakukaribishwa mazishini, kwa kuwa yeye ni miongoni mwa wasaliti wa nchi ya Uganda.
Baadhi ya waombolezaji waliwatishia kuwaua wabunge hao kama wasingeliondoka kwenye mazishi hayo.
Kutokana na kadhia hiyo, Mpuuga alimsogeza Kakooza karibu na kiti chake ili kumlind.
Nae waziri mkuu wa Baganda Charles Peter Mayiga alijaribu kuwatuliza wananchi hao ila juhudi zake hazikuzaa matunda, na hivyo walinzi wa Mayiga kulazimika kulazimika kutoa msaada wa kumuondoa Kazooka mazishini hapo ili asidhuriwe.