Na mwandishi wetu
Kamati ya ulinzi na usalama wilayani Manyoni, mkoani Singida imepanga kuwaondoa wananchi wote wanaoishi karibu na eneo la pori la Akiba la Muhesi ambako wamekuwa wakichimba visima na kuleta athari kwa tembo.
Mkuu wa kanda wa kikosi dhidi ya ujangili(KDU) wilayani humo Keneth Sanga anasema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na miezi ya hivi karibuni kuwepo kwa tembo wengi ambao waamekuwa wakitumbukia kwenye visima hivyo wakati wanapita maeneo hayo ya watu kwenda kutafuta malisho na maji.
Mkuu huyo anasema kuwa mpaka sasa takribani tembo 11 walitumbukia kisimani wakiwa wanapita eneo hilo na hiyo ni kutokana na hali ya ukame.

Katika tukio la awali kwenye kijiji cha Doroto kitongoji cha Mwakitanda, tembo wa tano walitumbukia kisimani ambapo wanne waliokolewa na mmoja kufariki dunia.
“Mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa kiongozi wa post ya Rungwa iliyopo Doroto kikosi kilishirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri ya Itigi na askari wa kituo hicho tuliomba na kupatiwa mtambo kutoka kwa kampuni ya wachina waliojenga barabara ya Manyoni-Tabora ambao walitupatia mtambo na kuweza kuwaokoa tembo wanne na tembo mmoja mdogo alikufa,” alisema Sanga.
Na huko katika kijiji cha Itagata wilayani humo, tembo watano walitumbukia ambapo wanne kati yao waliokolewa na maafisa wa wanyamapori wa halmashauri ya Itigi na mmoja kufariki dunia kutokana na kukanyagana wakiwa kisimani.
Sanga anaendelea kusema kuwa siku nyingine katika tarafa hiyo hiyo ya Itagata, tembo mmoja alitumbukia kisimani na kuokolewa.
Zoezi hilo limepangwa kufanyika kati ya Octoba na Novemba mwaka huu ambapo litafuatiwa na kufukiwa kwa visima hivyo ili kuondoa uwezekano wa tembo kutumbukia.