Na Hasna Ally
Inaelezwa kuwa ukiwekeza elimu kwa mtoto wa kike kuna mafanikio makubwa yenye manufaa ndani yake.
Kauli hiyo inadhihirishwa na usemi usemao, “ukimsomesha mtoto wa kike, utakuwa umeelimisha taifa nzima”.
Ni kwa msingi huo ndipo zikaanzishwa taasisi na mashirika yasiyo ya Kiserikali(NGOs) kwa ajili ya kumuwezesha mtoto huyo wa kike katika masuala mbalimbali ya kijamii ambayo amekuwa akikabiliana nayo.
Miongoni mwa taasisi hizo ni kama chama cha waandishi wa habari wanawake(TAMWA), TGNP-Mtandao, Msichana Initiative nakadhalika.
Taasisi na mashirika hayo yamekuwa yakijikita katika kupigania haki ya elimu kwa mtoto wa kike ambae amekuwa akiikosa kwa miaka mingi kutokana na mfumo wa jamii kumkandamiza.
Pia yamekuwa yakifanya kampeni za kuinua na kupaza sauti ya mtoto wa kike kwa kuwapatia elimu ya kutambua haki zao za msingi ikiwemo elimu ya jinsia, kijitambua pamoja na kushiriki katika mambo yatakayowajenga kiroho na kiakili ili kuongeza mariifa wawapo katika mazingira tofauti.
Hatua kama hizo kabla zilikuwa mithili ya ardhi yenye ukame isiyootesha mmea wowote ule lakini kwa sasa hali inabadilika na kuwa kama ardhi yenye rutuba yenye kuotesha mimea ya kustawi na kunawiri na kuleta matumaini.
Mfano wa picha halisi wa juhudi hizo kwa hapa nchini ni kwamba kumekuwa na wimbi kubwa la wanawake wasomi na viongozi wenye kutetea haki za mtoto wa kike. Kuna mama Samia Suluhu Hassan, makamu wa rais wa kwanza wa kike wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuongeza nguvu za kupigania haki ya kumkomboa mtoto wa kike kielimu. Na hiyo ni miongoni mwa kauli yake kuwa elimu ni kati ya vitu vya msingi kwa maendeleo ya mwanamke na ni kati ya masuala muhimu ambayo serikali imewekea mkazo.
“Kuliwa na vikwazo vingi vilivyoturudisha nyuma(wanawake) kama vikwazo vya ukosefu wa elimu,” alisema Mama Samia Suluhu Hassan.
Katika utafiti uliofanywa Januari ya mwaka 2016 na Shirika la Afya Duniani (WHO ), lilitaja Tanzania kuwa ni kati ya nchi tatu barani Afrika kwa ndoa na mimba za utotoni kwa asilimia 28.
Hali hiyo iliyambatana na wasichana wengi kuacha shule kwa changamoto mbalimbali pindi wanapokuwa katika safari yao ya kupata elimu na kushindwa endelea kupata elimu kabisa.
Kwa upande wake Serikali ya Tanzania bado imejiwekea mikakati na kuendeleza jitihada za kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu na kupunguza ukatili kwa mabinti kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Katika suala la kutia hamasa naye Waziri wa afya, maendeleo ya jamii jinsia, wazee na watoto, Ummy Ally Mwalimu hayuko nyuma kuhakikisha haki ya elimu kwa mtoto wa kike.
Katika moja ya hotuba zake, Waziri Mwalimu alisema, “Serikali imezingatia usawa katika usaili wa wanafunzi kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo.”
Inaelezwa kuwa, siku zote maendeleo huanza ndani ya jamii husika, Je katika suala la kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora jamii ina mchango gani?
Kujibu swali hilo, Caren Tengelemu, mwalimu wa shule ya msingi Kisukuru iliyopo Tabata Dar es Salaam, anasema, kwa upande wao wao kama walimu nambao ni watu waliomo ndani ya jamii ni wenye kuitikia wito kwa kuwapa wanafunzi elimu inayostahili.
Ila anasisitiza kuwa uwepo wa ushirikiano mzuri na wazazi huleta maendeleo bora ya kimasomo kwa wanafunzi wote hasa kwa mwanafunzi wa kike
“Wananchi kwanza wanapaswa kutambua elimu kwa mtoto wa kike si kwa maendeleo yake binafsi tu bali inauwezo wa kusambaa kwa kila mtu endapo watatilia mkazo,”alisema Mwalimu Tengelemu.
Kwa ujumla, maendeleo huonekana kwa macho kuliko mipango, malengo makubwa ya taasisi zinazojihusisha na haki za wanawake na watoto ni kutaka kuona jinsia ya kike inapata haki sawa na jinsia ya kiume hasa katika elimu, ajira, na sehemu zinginezo.
Ili kulifanikisha hili kwanza ushirikiano na umoja kwa wanawake wenyewe ndiyo nguzo imara itakayo fanikisha malengo hayo, pia kwa wanaume au wazazi wa kiume nao wanapaswa kutambua haki za mtoto wa kike ni zipi ili kuepuka ukatili wa jinsia kwa watoto, mimba pamoja na ndoa za utotoni.
Vilevile serikali nayo ina wajibu wakuweka utaratibu wa kuwepo na mazingira mazuri na salama ya kusomea kwa mtoto wa kike ili kujenga jamii ya wanawake wenye nguvu ambao wanauwezo wa kujitegemea na kufikia na ndoto zao walizojiwekea.